Uzima Milele Watoto

Yesu anawataka watoto wadogo waje kwake,
kwa maana ufalme wa Mbingu ni wao. Karibu Uzima Milele Watoto tujifunze pamoja.

Yusufu na Ndoto ya Farao

Hapo zamani za kale, Farao wa Misri aliota ndoto mbili za ajabu: kwanza, ng'ombe saba wanono waliliwa na ng'ombe saba waliokonda; pili, masuke saba manene yalimezwa na masuke saba membamba. Hakuna mtu aliyeweza kutafsiri ndoto hizo, hadi Yosefu, kijana wa Kiebrania gerezani, alipoitwa.

Yusufu alieleza kuwa ndoto hizo zilimaanisha miaka saba ya mavuno mengi itakayofuatiwa na miaka saba ya njaa kali. Alimshauri Farao kuhifadhi chakula wakati wa mavuno. Farao alivutiwa na hekima ya Yosefu na akamteua kusimamia mpango huo.

Mpango huo uliokoa Misri na mataifa jirani kutoka kwa njaa, na hekima ya Yusufu ilidhihirisha baraka za Mungu kwake.

Mafundisho: Hekima na unyenyekevu, Matumaini katika changamoto, Maandalizi kwa siku zijazo,Kuzingatia vipaji vya wengine na Umuhimu wa kujituma na uadilifu.

Elisha na Chungu cha Sumu

Hapo zamani, Nabii Elisha alienda mji wa Gilgali na kuwafundisha wanafunzi wa manabii. Siku moja, mwanafunzi mmoja alitoka kutafuta mboga, akakuta mti wa matunda asiyoyajua, akayachuma na kuyakata kata ndani ya chungu.

Chakula kilipokuwa tayari, kila mtu alipakuliwa, lakini walipoonja wakagundua chakula kile kilikuwa na sumu. Wakaogopa na kusema: "Kifo kiko kwenye chungu, hatuwezi kula!"

Elisha akaagiza aletewe unga, akautia ndani ya chungu na kusema wanywe tena. Walifanya hivyo, na mara chakula kikawa salama kabisa.

Funzo: Mungu anaweza kubadilisha jambo lolote baya katika maisha yetu na kulifanya kuwa lenye manufaa kwetu.

Yesu Alilisha Watu Elfu Tano

Yesu alipenda kufundisha Neno la Mungu, na siku moja alifundisha mkutano mkubwa wa watu maelfu. Ilipofika mchana, alimuliza Filipo: "Tutapata wapi chakula cha kuwalisha watu hawa? "Filipo akajibu: "Hata pesa hazitatosha kununua chakula cha kila mtu."

Andrea, aliyekuwa akisikia mazungumzo hayo, akasema:"Kuna mtoto hapa mwenye mikate mitano na samaki wawili."Yesu akasema wamlete huyo mtoto.

Yesu akachukua mikate na samaki, akaangalia juu mbinguni, akashukuru na kumuomba Mungu awabariki. Kisha akawagawia watu chakula hicho. Watu wote walikula hadi kushiba, na walipomaliza, Yesu akawaambia wanafunzi wake waokote vipande vilivyobaki. Walikusanya vikapu 12 vya mabaki!

Funzo: Yesu alitenda muujiza mkubwa kupitia kidogo kilichotolewa kwa imani. Hii inatufundisha kuwa Mungu anaweza kuzidisha chochote tunachompa kwa moyo wa ukarimu.

Eliya na Mwanamke wa Serepta

Mungu alimuagiza Eliya aende Sarepta, ambako alikutana na mjane aliyekuwa na kiasi kidogo tu cha unga na mafuta. Alimwomba maji na mkate, lakini mjane huyo akasema hiyo ilikuwa chakula chake cha mwisho kwa ajili yake na mwanawe. Eliya alimwambia asihofu, bali atengeneze mkate kwanza kwa ajili yake, akiahidi kuwa Mungu angesababisha unga na mafuta visipungue mpaka mvua itakaponyesha. Mwanamke huyo alitii, na kwa maajabu ya Mungu, chakula chake hakikupunguka hadi mwisho wa ukame.
Funzo: Mungu ndiye mpaji wa vyote, na hatatuacha tukihitaji tunapomwamini.

Mtoto wa mama wa Serepta Afufuliwa

Mtoto wa mama mjane wa Sarepta aliugua vibaya na hatimaye akafariki, jambo lililomwacha mama huyo katika huzuni kubwa. Akiwa amekata tamaa, alimlaumu Eliya kwa kufikiri kwamba kifo cha mtoto wake kilikuwa adhabu kwa dhambi zake.

Eliya alimchukua mtoto huyo juu ghorofani, akamlilia Mungu kwa maombi ya dhati, akimwomba arejeshe uhai wa mtoto. Eliya akajinyoosha juu ya mtoto mara tatu, na Mungu alisikiliza maombi yake. Uhai wa mtoto ukarejeshwa, na Eliya akamrudisha kwa mama yake.

Mama huyo, akiona muujiza huo mkubwa, alisema:
"Sasa najua hakika kuwa wewe ni mtu wa Mungu, na neno la Bwana kutoka kinywani mwako ni kweli."

Fundisho: Mungu ana nguvu za kushinda mauti na kurejesha uhai. Maombi ya unyenyekevu na imani yanaweza kuleta miujiza, na hadithi hii inaonyesha jinsi Mungu anavyowajali wanyonge na kuwatendea mema kupitia watumishi wake.

Kisa cha Hana na Eli

Hapo zamani za kale katika mji wa Rama. Kulikuwa na mwanamme mmoja aitwaje Elkana aliyekuwa akiishi na mke wake, Hana. Pamoja na mibaraka mingi waliyokuwa nayo Hana hakuweza kuwa na mtoto. Kila mwaka Elkana alipeleka familia yake Shilo kwa kuhani Eli kwa ajili ibada na sadaka. Siku moja Hana alifanya maombi ya kupata mtoto na kuweka nazili kwa Mungu. Kisha wakarudi nyumbani wakiwa na furaha wakiamini ya kuwa Mungu atawajibu ombi lao. Baada ya muda mchache Hana alipata mimba na kufanikiwa kujifungua mtoto wa kiume, aitwaye Samweli (nimemuomba kwa Mungu). Baada ya Samweli kuacha kunyonya Hana alimpeleka Shilo Hekaluni kwa Eli na kufanya ibada kisha akamuacha kama ilivyokuwa agano lake na Mungu.

FUNDISHO:

  1. Mungu hujibu maombi.
  2. Watoto ni mibaraka kutoka kwa Mungu hivyo twapaswa kuwakabidhi kwake

Fungu Lililo Jema

Kisa cha Mariam wa Bethania, kinaelezea watoto watatu (Lazaro, Martha na Mariam) waliokuwa wakiishi pamoja kwa upendo na amani. Siku moja Yesu aliwatembelea, Martha alitamani kumuudumia Yesu kwa Chakula na maji, Yesu alikataa lakini Martha akaenda kumuandalia. Lakini Mariam alibaki na kuketi miguuni pa Kristo na kupokea mafundisho, sisi kama watoto tuchague kuketi miguuni kwa Kristo ili tuweze kujifunza neno lake kama vile upendo, utii, adabu, kujitoa na kuwasaidia wenzetu.

Samueli Aitwa na Bwana

Kisa hiki tunapata hadithi ya Samueli aliyekuwa anaishi na Kuhani Eli, hekaluni. Kuhani Eli alikuwa ni mzee sana hivyo alikuwa akimuagiza shughuli mbali mbali. Siku moja Samueli akiwa amelala alisikia sauti ikimuita Samueli, Samueli alijuwa kuwa kuhani ndo anamuita, kisha akakimbia kwenda kwa kuhani, kuhani akamwambia sio yeye aliemuita kisha akamuelekeza kurudi kulala. Alipolala tena alishitushwa tena na sauti ikimuita Samueli ,Samueli akakimbia kwa kuhani, kuhani akasema sio yeye aliemuita akamrudisha tena kulala. Kwa mara nyingine akasikia sauti ikimuita tena kisha akakimbia kwa kuhani, safari hii kuhani akatambua kuwa ni Mungu ndiye aliyekuwa anamuita Samueli. Nae kuhani Eli akaamwambia Samueli, "ukisikia sauti ikikuita useme: Nena Bwana kwa kuwa mtumishi wako anasikia". Kisha akamuelekeza Samueli akarudi kulala. Kwa mara nyingine akasikia sauti ile kisha ikimuita kisha akafanya jinsi alivyo elekezwa na Kihani Eli, nae Mungu akampa ujumbe wake.

Yesu Amponya Kipofu

Kisa hiki kinaelezea nguvu za Mungu za uponyaji kwa kijana aliyezaliwa kipofu aliyeishi Yerusalemu. Yesu alimponya kwa kumpaka tope machoni alilolitengeneza kwa mate na udongo, kisha akamwambia kipofu akanawe katika kijito cha Siloamu. Baada ya kunawa akawa kaona.

Uumbaji

Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi.  Siku ya kwanza, aliumba nuru ili ikamulike giza nene.  Siku ya pili akaumba anga.  Siku ya tatu akaumba nchi kavu na kuotesha vitu vyote mfano miti mimea vipendezoa nchi.  Siku ya nne akaumba jua, nyota pamoja na mwezi ili vipate kumulika mchana na usiku.  Siku ya tano aliumba ndege wanaoruka angani pamoja na samaki.  Siku ya sita aliumba wanyama wa aina zote pamoja mwanadamu wa kwanza Adam na kumpa rafiki yake Hawa.  Siku ya saba akapumzika na akastarehe na kuitakasa siku ya saba (sabato).

Habili na Kaini

Kaini na Habili walikuwa ni ndugu, watoto wa Adam na Hawa.  Kaini alikuwa mkulima na Habili alikuwa mchunga kondoo.  Kaini akamtolea Bwana sadaka ya mazao na Habili akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake.  Bwana akakubali sadaka ya Habili, lakini ya Kaini akaikataa.  Kaini akaona wivu na kumuua nduguye Habili.  Bwana Mungu akamuuliza Kaini, “ndugu yako yuko wapi?” Kaini akajibu, “kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”  Ndipo Bwana akamwambia “umelaaniwa wewe na kizazi chako chote” na akamfukuza mbele ya uso wake na kusema atakayemuua Kaini atalipizwa mara saba kisasi.  Kaini akaondoka mbele za uso wa Bwana na kuelekea nchi ya nodi mbele ya edeni.

Nuhu na Safina

Mungu aliangalia dunia na kuona machafuko mengi, na ndipo akamwagiza Nuhu ajenge safina kwakuwa ataisafisha nchi kwa maji.  Nuhu akajenga safina akishirikiana na watoto wake na marafiki zake.  Alipomaliza kujenga, aliwahubiri watu kwa miaka mia na ishirini ili waingie ndani ya safina, lakini pamoja na kuwahubiria hawakuingia.  Mwishowe akaingia yeye pamoja na familia yake na wanyama wawili wawili, makundi saba ya wanyama safi na makundi mawili ya wanyama najisi. Baada ya kuingia kwenye safina, malaika wa Mungu akafunga mlango.  Mvua ikanyesha sana na watu wakamlilia Nuhu ili awafungulie lakini Nuhu aliwambia Bwana ndo amefunga mlango.  Mvua ilinyesha kwa siku arobaini na baada ya miezi saba Nuhu, familia yake na wanyama waliokuwa kwenye safina ndio walipona.  Kisha Nuhu akamtolea Bwana sadaka ya shukrani.  Mungu akatoa upinde wa mvua kama ishara kuwa hatoangamiza ulimwengu tena kwa maji.

 

Ibrahim na Isaka

Ibrahim alikuwa ni rafiki yake Mungu.  Mungu alitaka kujua kama Ibrahim anampenda kweli.  Mungu akamwambia Ibrahimu amtoe mtoto wake wa pekee, Isaka, kama sadaka.  Ibrahimu alikubali lakini aliwaza njiani kuwa huyu ni mtoto wake wa uzeeni na atamwambiaje mkewe Sarah, lakini hakujali akasema moyoni mwake nitamtolea Bwana sadaka.  Walipokaribia eneo la kutolea sadaka, Ibrahimu akawaambia wafanyakazi wake wabaki, naye akapanda na Isaka katika eneo la madhabahu, mlimani.  Walipokuwa wakipanda Isaka akamwuliza, “baba tuna kuni na moto lakini mwanakondoo yu wapi?” Ibrahimu akajibu, “Bwana atajipatia”. Walipofika madhabahuni alipanga kuni, akamfunga mwanae na kumweka juu ya madhabahu.  Lakini, alipoinua mkono ili kumtoa mwanawe mpendwa Isaka kama kafara, ghafla sauti ya Bwana ikasikika ikisema “usimtoe mwanao sasa nafahamu ya kuwa unanipenda kweli, tazama yule pale mwanakondoo.” Imetupasa kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote kuliko kitu chochote.

Wana wa Israeli na Bahari ya shamu

Musa aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri kuelekea Kanani wakiwa na familia zao pamoja na wanyama wao, lakini njia yao ilijawa na milima na mabonde, kwa mbele wakaona bahari, na mara kugeuka nyuma wakaona jeshi la Farao likiwafata.  Wana wa Israeli wakaogopa sana wakamlilia Musa, Musa akawambia: “msiogope, leo mtaona Mungu atakavyowaokoa”.  Ndipo Bwana akamwambia Musa ainue fimbo juu na kuinyoosha juu ya bahari ili maji yagawanyike, na maji yaligawanyika mara mbili na wakapita salama huku jeshi la farao likiwa linawafuata.  Kisha Musa akayaamuru maji na yakarudi huku yakilizamisha na kuliangamiza jeshi la Farao.  Wana wa Israeli waliashangilia  na kuimba nyimbo za ushindi.

Msamaria mwema

Bwana Yesu akiwa anafundisha alitokea Mwanasheria akimjaribu akamuuliza, “nifanye nini ili niweze kurithi uzima wa milele?” Yesu akamjibu “imeandikwa nini katika torati?”  Akajibu, akisema, “mpende jirani yako kama nafsi yako yote”. Mwanasheria akauliza “je, jirani yangu ni nani?” Yesu akamjibu; “Mtu mmoja akitokea yeriko kuelekea Yerusalem akaangukia kwenye mikono ya wanyanganyi, wakamvua nguo na kumtia majeraha.  Akatokea kuhani, akapita kando na mlawi nae akapita kando, lakini msamaria alipita na kumwonea huruma na kumpeleka nyumba ya wageni na kumpa dinari mbili mwenye nyumba ili amtunze.”  Yesu akamuuliza mwanasheria “kati ya hao, yupi alikuwa jirani yake?” akijibu, “ni msamaria”.  Akamwambia na wewe kafanye vivyo hivyo.

Image
Makazi
Dar-Es-Salaam, Tanzania
Namba ya simu
0764504284
Barua Pepe
info@uzimamilele.or.tz
Maswali na Majibu
 
Hatimiliki © Uzima Milele 2025. Haki zote zimehifadhiwa.

Search